1. Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali

Babu alipokaribia kukata roho, alimwita baba akamwambia, ‘Mwanangu,nitokako ni kurefu na nendako ni kufupu.’

        Kabla hajamaliza, baba alimkatiza na kumwambia, ‘Mbona wasema kwa huzuni, baba, una maana gani?’

Babu aliendelea, ‘Nilizaliwa yapata miaka mia moja iliyopita, lakini kifo ni pua na mdomo, ndiyo maana nimekwita nikupe buriani.’

        Papo kwa papo baba alipaliwa na pumzi asiweze kupumua wala kunena. Akajaribu kumbwagia jicho babu, lakini haikuchukua nukta kabla mboni za macho hazijaacha kuogelea katika chemchemi ya machozi. Babu alipoona mambo yamekuwa hayo, aling’amua kwamba akiendeleakuzungumza na baba bila mashahidi, wasia wasia wake haungepata hifadhi yoyote kwani mzee wangu hangeyapata yote ambayo yangeponyoka kutoka kinywani mwa babu. Ndipo alipokata shauri kumwambia baba atwite sisi sote. ‘Kina baba! Kina baba! Hebu njooni haraka,’ alitamka mzasi wetu, ‘Babu yenu anawahitaji hivi punde’, alimaliza.

        Kwa vile hali ya babu iliendelea kudhoofu, mwito wa ghafla namna ile ulitutia kiwewe.Sote tuliya bwaga majembe tukavisukuma kando viserema na kuzitupilia mbali fagio kwani tulikuwa katika hekaheka ya kurasharasha uwanja wa mji na kupalilia minyanya na mboga zingine. Tulipachika fulana au shati zilizokuwa karibu, tukalifuta jasho kwa viganja vya mikono yetu michafu. Hakuna hata aliyefikiria kukumbilia uani kwenye maji na taulo, wakati haukuruhusu. Tulijua ya kwamba leo ni leo, mwamba kesho ni mwongo. Kufumba na kufumbua tulijiona tupo matendeguni pa kitanda cha babu.

        ‘Wajukuu zangu! Nimewaita ili niwape mkono wa kwaheri. Kama mjuavyo, mbio za sakafuni huishia ukingoni, basi ukingo ndio huu. Hivi ndiko katika hali ya kufunganya; safari imewadia. Huenda nikang’oa nanga hata hivi leo; pengine hivi sasa. Dunia ni hadaa, ulimwengu ni shujaa.’

        Nikamwuliza, ‘Babu mbona watusemea kwa mafumbo? Hatulielewi wala hatulitambui ulilotuitia, nawe umekazana na vitendawili na mafumbo yasiyo kikimo.’ Baba yetu akasema, ‘Babu yenu yuahisi kwamba yuko karibu kukata roho, kwa hivyo amewaita ili aje awausie.’ Tukasema sote kwa sauti moja, ‘Alaa’.

        Babu akaendelea, ‘Nawaomba muishi kwa furaha kama mlivyoishi tangu mlipozaliwa. Mumtii mzazi wenu na muwe na bidii, mjiepushe na maovu ya dunia kama kuiba, kupigana, kusengenyana, kulaumiana nakijicho. ‘Na wewe,’ akamgeukia kitinda mimba chetu, Mwanamize. ‘’Jitafutie mvulana mzuri, mwenye busara na upendo na mwenye bidii, akuoe. Usiangukie mikononi mwa makurumbembe wasiokuwa na asili wala fasili; wasiojishughulisha kuchuja na kutengam mema kutoka kwa mabaya, wasio na adabu wala heshima. Na ukienda kwa mji wa watu, uwe na sifa ya hapa utokapo; watu wajue kwamba mjukuu wa marehemu Fulani ni mke kweli kweli, mlezi mwema, mwaminifu.’

        Akatugeukia sisi, ‘Na nyinyi, mtafute wake watiifu, wajuao watendalo, muwatunze, muishi ya raha hata nanyi mkongoke kama hivi nilivyokongoka mimi. Amina.’

        Baada ya kusema hayo, babu alitueneza mikono na mara akakata roho akafariki.

Maswali:

a) Pendekeza kichwa kifaacho taarifa hii.

b) Babu yuko katika hali gani kimaisha? Tetea jibu lako kwa kutoa sababu

ch) Tambua na uelee mbinu za kisanaa zilizotumiwa katika taarifa hii.

d) Eleza hisia anazozipata msomaji wa taarifa hii.

e) Mwandishi ametumia toni ipi katika taarifa hii.

f) Tambua mafunzo matatu unayoyapata kutoka taarifa hii.

 

2. Soma shairi lifuatalo kasha ujibu maswali.

        Mja si mwema

1

Mkono inuka

Upate ya’ ndika

Ipate someka

Wapate yahika

inuka hima

kwa khati njema

wenye kusoma

na kuyapima

twaa kalamu

hino nudhumu

waifahamu

yaliyo humu

2

Kuandika anza

Na mimi naanza

Alivyonifanza

Wapate jitunza

anza ‘sikawe

kisa chenyewe

nao wajuwe

salama wawe

mkono wangu

cha mlimwengu

waja wenzangu

hawa ndu zangu

3

Mja sikudhani

Nikamuamini

Kumbe mwafulani

N’ shambani

sikudhaniya

hafikiriya

hakuzoweya

ingawa baya

‘tanizunguka

Hatageuka

Kuaminika

lishanifika

4

Menitenda kisa

‘Mezinduka sasa

Ni yangu makosa

Sikuwa napasa

kisa adhimu

n’shafahamu

najilaumu

hata sehemu

mja mcheni

najuwa kwani

kumuamini

kumthamini

5

‘Meniuwa mja

Mjaye daraja

Muonapo mja

Asije akaja

Mja ni nduli

Nda kikatili

Kaani mbali

(kwani habali)

Tahadharini

Hana imani

Mujitengeni

Kuhasirini

6

Mja hana haya

Mja ni mbaya

Na ukisha ngiya

Mmoja kwa miya

Baya hazimo

Hutimba shimo

Azome zomo

Ndiye hayumo

Mwake usoni

Ungiye ndani

Furaha gani!

Baya kundini

-10 Januari, 1971

Maswali:

a) Shairi hili linahusu nini?

b) Tambua na ujadili matumizi ya mbinu za inkisari na mazda

ch) Tambua aina ya shairi hili na utambue istilahi zinazotumiwa kueleza kila kipande.

d) Kwa kurejelea shairi hili, eleza ikiwa mshairi ni mwananmapokeo au mshairi huru

e) Jadili matumizi ya mbinu za kisanaa zilizotumiwa

f) Fafanua toni ya shairi hili.

g) Changanua mafunzo unayoyapata kutoka shairi hili

4. Rejelea shairi lolote katika diwani ya Abdilatif Abdalla lenye maudhui ya uvumilivu na ueleze:

a) ujumbe uliomo,

b) hisia za mwandishi,

ch) mafunzo yonayopatikana humo

 

3. Soma taarifa ifuatayo kasha ujibu maswali yatakayofuata

MITANDAO

Dunia ilivyo sasa sivyo ilivyokuwa karne moja iliyopita. Hata tukizingatia kipindi cha hivi majuzi, maisha yalivyokuwa miongoni miwili mitatu iliyopita ni tofauti kabisa na ilivyo sasa. Kasi ambayo dunua inakimbia hivi leo imezidi kiasi, huenda ikapata ajali mithili ya treni na sisi abiria tukaangamia au kujeruhiwa vibaya. Kama moto uliomwagiliwa petrol, mamba mapya huibuka kila kuchao kama ndimi za huo moto. Ile kasi iliyotajwa imedhihirika wazi zaidi katika uvumbuzi wa kisayansi na maendeleo ya teknolojia.

        Mabadiliko yasiyo na mshabaha yalitoa nanga ile siku ambayo mtandao wa intaneti uliposhika hatamu na kuupindua kabisa uwanja wa mawasiliano. Ikatokea kwamba kuandikia mtu barua kwa wino na karatasi ni kitendo cha jana. Huduma za posta zikaanza kuwa kisa-asili kihadithiwacho watoto na nyanya yao jioni.

        Mtandao ukaziburura huduma zingine za barua pepe na kurasa za mawasiliano ya kijamii, mathalani ‘facebook’na twitter’. Tovuti zingine kama vile ‘yahoo’ na ‘google’ zikatawala mawasiliano na kupenya kila mahali kutoka ofisi hadi sebule na hatimaye kutua katika vyumba vya malazi.

        Vijana kwa wazee waliparamia hili lori la maendeleo ya teknolojia lisilobagua rangi, jinsia, dini hata umri. Asiyelipanda lori akaachwa gizani, mshamba kabisa! Vijana wakajiita kizazi cha ‘dot.com’ nakuwabandika wazee wao kizazi cha ‘S.L.P’

        Mtandao ukawa fumbo. Ukabatilisha biashara nyingi na wenyewe wakarudi makwao kushika jembe waliloliasi misimu kadha iliyokuwa imepita. Mkondo wa utendaji shughuli ukabadilika. Mtumishi wa posta akastaafu mapema, mchuuzi wa bahasha za rangi akafunga duka. Kompyuta zikageuza mambo, zikatoka mezani na kuhamia begani, kisha kutoka begani sasa zashikwa viganjani, zapapaswa tu.

        Aliyedhani papo hapo teknolojia imepumzika hakuwa na habari juu ya tufani iliyomjia. Simu za mkononi,yaani rununu, zikapanua matumizi. Atakaye gazeti, muziki, kitabu, chochote alifungua tu simu na kukipokea pale pale alipo. Wakati tukistaajabia haya, mtandaoni. Aliyezoea kukaa kitako, mguu kauweka juu ya mwingine akiwasubiri wateja kuingia duka alibakia mfuko mtupt, akizitazama bidhaa zake nazo zikamttazama. Kumbe wateja washampita nyuma, tayari washampita nyuma, tayari washatoka kwenye ‘line’ na wako ‘online’, wanapapasa vifaa na kununua kwa kutumia vidole, popote walipo. Ofisini, mkutanoni, matangani, kanisani, hospitalini, hata chooni, kokote, popote.

        Mtandao ukawa mtandao, wakausifu, wakaukashifu! Waja wenyewe, nduma-kuwili walivyo, wakaidhania dunia kuwa uwanja tambarare. Leo bwana Fulani karidhika kwa vile alivyonunua bidhaa bila kutoka kule aliko. Keshoye kalalamika kwa kugundua bintiye kachezewa na vulana lenye jina la ajabu alilokutana nalo kwenye ‘facebook’ baada ya kujuana kwa masaa mawili. Basi mtandao ukawa asali-chungu! Ile kasi inayorusha neon la Bwana kutoka Roma hadi Uganda ndiyo ileile inayorusha picha za uchi kwa nchi nzima.

        Papo hapo, ikabainika wazi kwamba dunia tunayoilaumu nayo ishapigwa bumbuazi ikitazama yale tunayoyatenda na kujitenda. Inaona kuwa ni mwiba wa kujichoma, na chambilecho wavyele, haitotwambia ‘pole’. Iulize dunia, “kwa nini yanayotokea yanatokea vile yanavyotokea?” Itakujibu, “mtandao ni zana kama vile nyundo, upanga, jembe. uitumiavyo vile utakavyo ukiwa tayari kuyakubali matokeo ya matumizi yako.” Tamthilia ya ulimi, mtandao ni zana iwezayo kujenga na kubomoa. Uzamuzi upo mikononi mwa mwenyewe.

Maswali:

a) Ni mabadiliko gani ambayo yametokea duniani katika miongo miwili iliyopita na ilichochewa na nini?

b) Kulingana na taarifa, ni huduma gani tatu ambazo zimekwama kwa sababu ya mtandao wa intaneti?

ch) Kwa kurejelea taarifa hii, jadili kwamba intanetini kama upanga unaokata kuwili

d) “Intaneti no zana, utumiavyo ndivyo ikupavyo.” Jadili ksuli hii huku ukirejelea taarifa yenyewe.

e) Eleza maana za kizazi cha ‘dot.com’ na cha S.L.P kama vinavyorejelewa katija taarifa.

f) Eleza maana za misemo ifuatayo kama ilivyotumiwa katika taarifa:

        i) …zikaanzakuwa kisa-asili,

        ii)…jembewaliloliasi,

        iii)…tufani iliyomjia,

        iv) Mtandao ukawa asali-chungu

        v)… ni mwiba wa kujichoma

 

MWINYI HATIBU MOHAMED: Malenga wa Mrima

4. Soma shairi lifuatalo kishaujibu maswali.

 UTII

Rai mwema ni Yule, aliyejaa utii
Si ubishi na kelele, akanywalo hasikii
Ni mwasi huyo jinale, achunguzwe kwa bidii
Raia asiyetii, ni fisadi wa nchiye

Uonapo uhalifu, usambe huuzuii
Ndiyo huo uvunjifu, kamawe huzingatii
Mwanachi mwadilifu, hilo halikadirii
Raia asiyetii, ni fisadi wa nchiye

Utii kama haupo, sheria haziagii
Imanihuwa haipo, na mema hayatujii
Usalama hufa papo, mara nchi ikadhii
Raia asiyetii, ni fisadi wa nchiye

Nia za watu watano, ambazo hazififii
Uchao ni tangamano, si chusa hawachukii
Hushinda kumi na tano, ambao hawatulii
Raia asiyetii, ni fisadi wa nchiye

Maswali:

a) Kwa kurejelea shairi hili, eleza sifa za raia mwema

b) Tambua na ueleze vipengele vya kisanaa vilivyotumiwa katika shairi hili

ch) “Nia za watu watano, ambazo hazififii

Hushinda kumi na tano, ambao hawatulii”

Mshairi anamaanisha nini katika mishororo hii?

d) Ni nini toni ya mshairi katika shairi hili?

e) Ni nini kusudi la mshairi?

f) Shairi hili linakufunza nini?

g) Eleza maana ya maneno haya kama yalivyotumiwa katika shairi hili

i) fisadi,

ii) hisa,

iii) uvunjifu

 

6. Kwa kurejelea diwani ya Mwinyi Hatibu Mohamed ya Malenga wa Mrima chambua shairi loote lenye maudhui ya uanadamu ukizingatia:

a) ujumbe,

b) hisia,

ch) toni,

d) mafunzo yaliyomo